Emma Stone ndiye mwigizaji wa kike anayelipwa pesa nyingi zaidi miongoni mwa waigizaji Duniani mwaka huu.
Mwigizaji huyo aliyeigiza katika filamu iliyovuma sana mwaka huu ya La La Land alilipwa $26m (£20m) katika kipindi cha miezi 12 kati ya Juni 2016 na Juni 2017, sana kutokana na ufanizi wa filamu hiyo.
Malipo hayo yalimfanya kuongoza katika orodha ya kila mwaka ya jarida la Forbes, na kuwashinda Jennifer Anniston na Emma Watson.
Emma alishinda tuzo ya mwigizaji bora wa kike Tuzo za Oscars mwaka huu kwa uigizaji wake kama Mia katika La La Land.
Mapato ya Emma yalipanda kwa 160% ukilinganisha na mwaka 2016, alipolipwa $10m (£8m).
Mwigizaji huyo wa miaka 28 alizungumzia kuhusu pengo la mishahara kati ya waigizaji wa kiume na wa kike, ambapo alifichua kwamba waigizaji wenzake wa kiume wameamua kwa hiari kupunguziwa mishahara ndipo walipwe kiasi sawa.
Mwaka huu, waigizaji wa kike 10 wanaolipwa pesa nyingi zaidi kwa pamoja walipata $172.5m (£134m), kabla ya kutozwa ada na ushuru.
Jennifer Aniston alikuwa wa pili baada ya kupata $25.5m (£20m), sana kutokana na kutumiwa kwake kuuza Smartwater, mafuta ya ngozi ya Aveeno na shirika la ndege la Emirates.
Emma Watson ndiye Mwingereza pekee aliyekuwa kwenye orodha hiyo ya 10 bora, akiwa katika nafasi ya sita.
Waigizaji hao wengine walikuwa ni Melissa McCarthy, Mila Kunis, Charlize Theron, Cate Blanchett, Julia Roberts na Amy Adams.
Dwayne "The Rock" Johnson aliongoza orodha ya waigizaji wa kiume Hollywood waliopata pesa nyingi $64.5m (£50m) kati ya Juni 2015 na Juni 2016.
Jennifer Lawrence na mwigizaji mwenzake Amy Adams walilipwa mishahara ya chini sana ukilinganisha na waigizaji wenzao wa kiume katika filamu ya American Hustle.