TANZANIA IMESHUKA KATIKA CHATI ZA UKARIMU DUNIANI



Ripoti Mpya ya Ukarimu ya Mwaka 2017 Iliyotolewa mwishoni mwa Wiki iliyopita inabainisha sasa Tanzania inashika nafasi ya 63 duniani kutoka 57 Mwaka jana, nyuma ya majirani Kenya na Uganda katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Tanzania Imeporomoka nafasi Sita katika utafiti wa Ukarimu Duniani ikiwa ni Mwaka Mmoja baada ya kufanya vizuri.

Katika Ripoti hiyo ya kila Mwaka inayoandaliwa na Asasi ya Kiraia ya Kimataifa kutoka Uingereza ya Charities Aid Foundation (CAF), inaonyesha Tanzania imeanguka katika vipengele viwili kati ya vitatu ambavyo hutumika kupima ukarimu wa watu wa nchi husika.

Mwaka jana, Tanzania ilifanya vyema katika utafiti huo katika vipengele vyote vya kumsaidia usiyemjua, kuchangia fedha na kujitolea muda kwa ajili ya kuwasaidia wale wenye uhitaji.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya nane, ni rahisi kwa Mtanzania kukupatia fedha lakini si kupoteza muda wa kukusaidia au kukuhudumia iwapo hakufahamu.

Katika ripoti ya mwaka huu, Tanzania inashika nafasi ya 110 katika kipengele cha kujitolea muda kwa wenye uhitaji na nafasi ya 60 kati ya 138 zilizofanyiwa utafiti Duniani katika kipengele cha kusaidia wageni wasiofahamika.

Ni kipengele kimoja tu cha kujitolea fedha ambacho Tanzania imepaa kwa nafasi 13 kutoka nafasi ya 49 mwaka jana hadi nafasi ya 36 mwaka huu ikiwa juu ya Uganda, Rwanda na Sudan Kusini.