CHUI ASIMAMISHA SHUGHULI KATIKA KIWANDA CHA MAGARI.

 
Unaambiwa, Chui mmoja amesimamisha shughuli katika kiwanda cha magari kilichopo India kwa takribani saa 36 tangu aonekane kwa mara ya kwanza siku ya Alhamis asubuhi kupitia Camera za CCTV katika idara ya injini iliyo na karibu ukubwa wa ekari 6 na kuonekana tena mara kadhaa baadaye.

Kiwanda  hicho cha magari ya Maruti Suzuki kilicho mji wa Manesar, usio mbali sana na mji mkuu Delhi ndicho kikubwa zaidi nchini India kinachounda karibu magari milioni 1 kwa mwaka.

Maafisa 12 wa wanyamapori na karibu polisi 50 walifika katika kiwanda hicho na kuwaambia  maelfu ya wafanyakazi waliowasili asubuhi, kusubiri nje wakati wakimwinda chui huyo.

Ilichukua muda wa saa kumi kumdunga dawa ya kumtuliza na kumkamata chui huyo. Baada ya chui huyo kudungwa dawa ya kumtuliza alishikiwa na kupewa matibabu kabla ya kurudishwa porini.

Visa vya makabiliano kati ya binadamu na wanyama vimekuwa vingi nchini India, ambapo makao ya wanyamapori yanazidi kudidimia na kuchangia ndovu na chui kuingia maeneo ya watu. Kuna takriban chui 12,000-14,000 nchini humo na takribani chui mmoja huuliwa kila siku.

Mwaka uliopita chui aliingia kwenye shule moja iliyo mji wa Bangalore nchini India, na kuwajeruhi watu 6 ambao walijaribu kumkamata.