MWANAMKE ALIYEKAA NYUMBANI KWA MIAKA 25 KUTOKANA NA UZANI MKUBWA AMEFARIKI DUNIA

Unaambiwa, Eman Ahmed Abd El Aty Mwanamke raia wa Misri ambaye aliaminiwa kuwa mtu mwenye Uzani mkubwa zaidi Duniani amefariki kwenye hospitali moja katika umoja wa Falme za Kiarabu.

Familia yake inasema kuwa alikuwa na uzani wa kilo 5 alipozaliwa kabla ya kupatikana na ugonjwa wa matende na Wakati alipofikisha umri wa miaka 11 Uzani wake uliongezeka maradufu na akaugua kiharusi ugonjwa uliomuacha kitandani kwa kipindi kirefu cha maisha yake.

Kabla hajafanyiwa upasuaji familia yake ilisema kuwa hakuwa ameondoka nyumbani kwake kwa miaka 25 na alikuwa amepelekwa nchini India kufanyiwa upasuaji wa kupunguza uzito wa mwili na iliripotiwa kuwa uzito wake ulipungua kwa kilo 300 kutoka uzito wa kilo 500.

Wakati akipelekwa India Kitanda alichosafirishwa nacho ni kitanda maalum kilichoundwa na mafundi wa Misri kwa kufuata matakwa ya shirika la ndege la Egypt Air Na Kilikuwa na mitambo na vifaa vya huduma ya dharura.

Bi. Abd El Aty alilazwa katika hospitali ya Abu Dhabi tangu mwezi Mei baada ya kuhamishiwa huko kufuatia upasuaji aliofanyiwa nchini India. Taarifa za hospitali zinasema kuwa mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 37 alikuwa na ugonjwa wa moyo na matatizo ya figo.