MAMBO YANAYOWEZA KUCHOCHEA MAFANIKIO YAKO.

Maisha yameghubikwa  na mambo mengi yanayofungamana na changamoto mbalimbali ambazo zinaweza kukwamisha au kuchochea mafanikio.
Haya ni baadhi ya mambo yanaweza kuchochea au kukwamisha mafanikio yako.

1. Mazingira.
Mazingira tunayoishi yana mchango mkubwa sana katika kuchochea au kukwamisha maisha ya mtu.

Mazingira yoyote uliyopo yana mchango mkubwa sana kwenye maisha yako, haijalishi huo mchango ni hasi au chanya. 
Kikubwa jifunze kuyatumia mazingira uliyonayo yakusaidie kufanikiwa hata kama ni mabaya. Kama upo kwenye mazingira yanakurudisha nyuma unatakiwa kutoka hapo haraka sana kwa kujitengenezea mazingira chanya ya kukusaidia kufanikiwa.

2. Matukio.
Hakuna ubishi pia matukio yana uwezo mkubwa wa kuathiri maisha yetu kwa kiasi kikubwa. Haijalishi matukio hayo ni hasi au chanya lakini yanauwezo wa kuathiri maisha yako. 
Mtu anapokabiliana na matukio chanya siku zote ni rahisi kujifunza kutokana na matukio hayo.
Pia mtu anapokutana na matukio hasi ni rahisi sana ubungo kuwa na mawazo ya kukata tamaa siku zote.


3. Maarifa.
Nguzo kubwa ya mafanikio imejikita kwenye maarifa. Watu wote wenye mafanikio, wana maarifa sahihi ya kuwasaidia kufanikiwa. Kutokuwa na maarifa ya kuweza kukusaidia kwenye maisha ni kama ujinga fulani hivi.

Watu wengi wanashindwa kufanikiwa kwa sababu ya kukosa maarifa muhimu ya kuwasaidia kufanikiwa. Wengi hawako tayari kutoa ujinga ulio kichwani mwao kwa kujifunza, zaidi hubaki kama walivyo. Kwa kawaida,  unapokuwa na maarifa bora ni rahisi kufanikiwa, lakini unapokuwa huna maarifa sahihi kufanikiwa inakuwa sio rahisi kabisa.

4. MATOKEO.
Mara nyingi sana tunaathiriwa na matokeo, iwe matokeo yetu binafsi, matokeo ya kijamii au ya kifamilia. Kwa mfano tunapokuwa tuna matokeo mabaya kwa mfululizo yawe ya kifedha, mahusiano mabaya na jamii au kifamilia matokeo hayo ni rahisi sana kuharibu maisha yetu kwa kuamini hiyo ndiyo sehemu ya maisha yetu.

Lakini matokeo yanapokuwa mazuri hiyo hutusaidia sana kujiamini na kujikuta tunatengeneza maisha yetu na kuwa bora zaidi.

 5. Ndoto zetu.
Kutokana na udogo wa ndoto tulizonazo hupelekea kuishi maisha mabaya ama kutokana na ukubwa wa ndoto tulizonazo hupelekea kuishi maisha ya mafanikio. Kitu cha msingi ni kutambua unataka nini katika maisha. Ukijua unachokitafuta ni rahisi sana kupambana na kufikia ndoto zako.

Kwa ujumla mazingira, matukio, maarifa na ndoto zetu tulizonazo, ni baadhi ya mambo yenye uwezo wa kuathiri maisha na malengo yetu kwa sehemu kubwa sana kuliko tunavyofikiri.

Tanguliza Mungu katika mambo yako kwani ndio njia ya mafanikio bora kwenye jambo lolote.